Pamoja na mambo mengine Rais ameamua kuunda Tume maalum ya Katiba, yaani Constitutional Review Commission. Tume hiyo itakayoongozwa na Mwanasheria aliyebobea, itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii yetu kutoka pande zetu mbili za Muungano. Jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote bila kubagua, vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wa nchi yetu kote nchini, katika kutoa maoni yao juu ya wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi yao. Baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi. Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika.