• Mnyika amshukia Ngeleja mikataba ya gesi, mafuta

    Geofrey Nyangóro
    MBUNGE wa Ubungo, John  Mnyika  ametaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kuwajibika kwa kitendo chake cha kuendelea kuruhusu kusainiwa kwa mikataba katika sekta ya madini bila ya kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusishwa.

    Mnyika ambaye pia ni Waziri kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini ametoa kauli hiyo jana, siku moja tu baada ya Waziri Ngeleja kutiliana  saini kwa niaba ya Serikali na kampuni ya kuchimba mafuta na gesi ya Swala.
    Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Mnyika alisema kasi ya uingiaji mikataba inayofanywa na Wizara hiyo bila ya kushirikisha Bunge ni hatari na kwamba hadhari inapaswa kuchukuliwa ili kuepusha uchumi wa nchi na haki za wananchi kuhujumiwa.

    “Tunapaswa kuchukua tahadhari juu ya kasi ya siku za karibuni ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake kuingia mikataba ya muda mrefu ya utafutaji wa mafuta na gesi asili katika maeneo mbalimbali nchini, hii itaepusha uchumi wa nchi na haki za wananchi kuhujumiwa,” alisema Mnyika na kuongeza;

    “Waziri  Ngeleja anapaswa kuwajibika kwa kuendelea kuruhusu kusainiwa kwa mikataba bila Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusika katika hatua za awali za maandalizi ya mikataba husika,” alisema.

    Mnyika alimtaka Waziri huyo mwenye dhamana katika wizara ya Nishati na madini kuueleza umma sababu za Serikali kuendeleza usiri wakati wa kuingia mikataba hiyo hata kwa wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi.
    Mnyika alionya kasi ya uingiaji mikataba bila uchambuzi yakinifu isipodhibitiwa kwa mwelekeo sahihi wa sera, sheria, mipango na usimamizi italeta athari kubwa katika usalama na uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

    Mnyika aliitaka  Serikali kusitisha shughuli za uingiaji mikataba mingine mikubwa ya madini, mafuta na gesi asili bila kuzihusisha Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya mikataba hiyo aliyodai ni mikubwa yenye maslahi mapana ya nchi na athari kwa wananchi wa maeneo mbalimbali.

    “Kwa utaratibu wa sasa kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ya mwaka 1988 pamoja na kanuni na taratibu za Bunge, kamati au mbunge anaweza kuomba kwa serikali kupitia kwa ofisi ya Bunge nakala ya mikataba baada ya kusainiwa,” alisema Mnyika na kuongeza ,

    Lakini, Katiba na sheria hazikatazi Bunge kuisimamia Serikali kuanzia katika hatua za awali za maandalizi ya mikataba badala ya kusubiri kuisimamia Serikali katika kutekeleza mikataba mibovu iliyoingiwa bila ushiriki wa wananchi au wawakilishi wao ambapo aliitaka wizara kutumia fursa hiyo kulinda masirahi ya umma.
     
    Katika hatua nyingine, Mnyika alimshauri Rais   Jakaya Kikwete kuiongoza serikali kufanya  marekebisho ya sheria za utafutaji na uzalishaji wa mafuta za mwaka 1980 na pia kuharakisha kutunga sheria ya gesi asili ambayo hadi sasa haipo.

    Serikali imengia mktaba na kampuni ya Swala na kufanya mikataba ya utafutaji mafuta na gezi kwa hapa nchini hadi kufikia juzi kuwa 26 kiwango kilichodiwa ni kikubwa kuliko nchi nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

    View more...

0 comments
Report